UNAIFIKIRIAJE Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, pale itakapogeuka kuwa kitovu cha vifaa vya elektroniki, ikitengeneza simu na kompyuta, ni Chunya ya kufikirika au halisi!
- Madini yanayotumika kutengeneza vifaa vya kisasa vya elekroniki kama vile simu na kompyuta. Wana Chunya wajihoji kama watafaidika
Kutokana na mfumo wa uchumi tuliourithi, ni wazi itaendelea kuwa kitovu cha malighafi ya madini yenye thamani kubwa duniani, lakini mabadiliko ya kimtazamo katika uchumi, yataibadili wilaya hiyo kwa kuifanya kuwa kweli ndoto ya Chunya kuwa kitovu cha viwanda vinavyotengeneza vifaa vya elektroniki.
Kwa takribani karne moja sasa Wilaya hiyo imehusishwa zaidi na utajiri wa dhahabu, lakini taarifa za hivi karibuni zinaibadili taswira hiyo, ni baada ya kugundulika kwa madini vito ama rare metals, yatumikayo katika vifaa vya eletroniki.
Haya ni madini muhimu sana katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa elektroniki, na Chunya inaorodheshwa miongoni mwa maeneo ya akiba kubwa ya madini hayo duniani kwa sasa.
Taarifa zilizopo kwenye tovuti ya Kampuni ya Peak Resources ya nchini Australia , iliyofanya utafiti wa madini hayo huko Ngualla wilayani Chunya, zinabainisha kuwa kiwango cha madini hayo ndicho kikubwa kugunduliwa duniani katika miaka ya hivi karibuni yakiwa ya daraja la juu.
Madini hayo yameitwa “rare earth metal” kutokana na hali ya uwepo wake ardhini ambapo yapo katika mchanganyiko na vitu vingine tofauti na madini mengine, kama vile dhahabu, almasi na shaba yalivyo, ambayo hupatikana yakiwa yenyewe.
Kugundulika kwa madini hayo ni habari njema kwa Taifa, lakini historia ya Wilaya hiyo kuhusu utajiri wake wa dhahabu, haitoi matumaini sana kwa wananchi wilayani humo, na swali linalowasumbua, ni je, Wilaya hiyo itaendelea kutajirisha wageni na kuendeleza miji ya nje, yenyewe ikibaki katika lindi la ufukara?
Uendelezaji mradi
Pamoja na kukamilika kwa kazi ya utafutaji madini hayo, shughuli za uchimbaji bado, na kuanza kwake itategemeana na upatikanaji wa fedha za mradi huo.
“Wako kutafuta fedha, kuanza kwa shughuli za uchimbaji hadi wapate fedha,” anasema Kamishina Msaidizi wa Madini, Wilfred Machumu.
Katika taarifa yao iliyopo kwenye tovuti yao, http://www.pekresources.com.au
External Links icon
Kampuni ya Peak Resources inabainisha kuharakisha utekelezaji mradi huo, wanaoutegemea kuwa wenye gharama ndogo na muda mrefu katika utekelezaji wake.
Kazi za awali, kama vile upembuzi yakinifu na uchambuzi wa kiuchumi (preliminary feasibility study – PFS and economic assessment), kwa mradi huo imekamilika.
Umuhimu wa rare earth metals katika maendeleo ya nchi
Miongoni mwa matumizi makuu ya madini hayo ni pamoja na kutumika katika utengenezaji wa vifaa mbalimbali vya elektroniki vinavyotumika katika maisha ya kila siku ya mwanadamu duniani. Vifaa hivyo ni kama vile, DVDs, mfumo wa kumbukumbu wa kompyuta, simu, balbu za umeme, betri na sumaku.
Kwa mujibu wa http://www.geology.com
External Links icon
mahitaji ya madini hayo duniani yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Mfano wa bidhaa moja tu, simu za mkononi, zimefika zaidi ya bilioni saba tofauti ya miaka 20 iliyopita ambapo zilikuwa chache sana.
Matumizi ya madini hayo kwenye utengenezaji kompyuta nayo yanaelezwa kuwa ya kasi sawa na takribani ile ile ya simu za mkononi.
Pamoja na matumizi hayo, madini hayo yanabainishwa kutumika pia katika ulinzi, ikiwemo kutengenezea vifaa mbalimbali vya kijeshi vya kielektroniki, ikiwemo vifaa vya mawasiliano, miwani ya usiku na GPS.
Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo Tanzania itayatumia madini hayo kuendeleza viwanda vya utengezaji wa vifaa hivyo au itaendeleza utamaduni wa kuuza nje malighafi, na kisha kuwa soko la vifaa hivyo vinavyotengenezwa na madini hayo yanayopatikana nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo hakuwa tayari kujibu swali hilo pamoja na lililohusu umiliki wa mradi huo, na badala yake alimwelekeza mwandishi kuwauliza Kampuni ya Peak Resources wenyewe.
“Wasiliana na Kampuni hiyo, ikupe majibu ya maswali yako,” alijibu Profesa Muhongo kwa ujumbe wake mfupi wa simu.
Majibu ya Waziri Muhongo yalitokana na maswali aliyoulizwa iwapo kuna mipango yoyote madini hayo kutumika hapa nchini kuendeleza sekta ya viwanda vya vifaa vya kielekroniki na umiliki wa mradi huo ulivyo.
Taarifa za Kampuni hiyo zinaonyesha kuwa mradi huo unamilikiwa na Kampuni hiyo ya Peak Resources kwa asilimia 100. Hata hivyo uongozi wa Kampuni hiyo ulipotafutwa kwa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu mradi huo haukuweza kupatikana.
Wakati Waziri Muhongo akielekeza waulizwe Kampuni ya Peak Resources, juhudi zote za kuwatafuta na kuwasiliana nao kwa njia ya mtandao, hazikufanikiwa. Walipotafutwa kwenye ofisi zao, katika Jengo la Golden Jubilee Tower lililopo kwenye Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, kama inavyoelekezwa kwenye tovuti yao, hawakupatikana.
Mmoja wa washirika wa Kampuni ya sheria ya CLYDE & CO, Michael Strain anakiri kampuni hiyo kupanga kwenye jengo hilo huko nyuma na kubainisha kwamba walihama lakini akiwa hafahamu walikohamia.
Pamoja na Strain kuwatumia ujumbe kwa njia ya mtandao kuwajulisha, uongozi wa kampuni hiyo haujajibu.
Ofisi za Madini Wilaya ya Chunya na Mkoa wa Mbeya, zote hazina taarifa zilipo ofisi za Kampuni hiyo hapa nchini.
Kampuni ya Peak Resources ilianza shughuli za utafutaji madini hayo huko Ngualla wilayani Chunya Septemba, mwaka 2009 na tangia wakati huo imejihusisha kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo na ya kijamii katika vijiji vilivyomo kwenye eneo la mradi.
Miradi iliyonufaika na misaada ya kampuni hiyo ni pamoja na ile ya elimu, zikiwamo shule za msingi na sekondari katika Kijiji cha Ngualla pamoja na maeneo mengine ndani ya wilaya hiyo.
Kampuni hiyo imejenga vyumba vya madarasa na kutoa madawati, vitabu, vifaa vya michezo, vitanda na magodoro, ukarabati wa barabara na usambazaji maji, pamoja na kusaidia matengenezo ya njia ya kurukia ndege wilayani humo.
Swali linaloumiza vichwa vya baadhi ya watu, ni jinsi gani madini hayo yatainufaisha wilaya ya Chunya na watu wake, au itakuwa hadithi ile ile ya kale, kuondoka na mali huku wananchi wakibaki na umasikini wao.
No comments:
Post a Comment