NI KUHUSU MAMLAKA
YA BUNGE MAALUM & RASIMU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA ILIYOWASILISHWA
KWENYE BUNGE MAALUM NA MWENYEKITI WA KAMATI YA UANDISHI YA BUNGE MAALUM
Tarehe 25 Septemba, 2014, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa
amri kuhusu maombi yaliyofunguliwa na Bwana Saed Kubenea, mwandishi
habari mwandamizi na mhariri wa gazeti la Mwanahalisi kutaka Mahakama
Kuu itoe ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge Maalum kwa mujibu wa kifungu cha
25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za nchi
yetu. Katika amri yake hiyo, Mahakama Kuu imesema yafuatayo kuhusu
mamlaka ya Bunge Maalum:
(a) “Kwamba kuna mgongano katika
maana ya maneno yaliyotumika kwenye kifungu cha 25 cha Sheria hiyo
kwenye toleo la Kiingereza la Sheria hiyo. Hata hivyo, licha ya mgongano
huo, tafsiri sahihi ya maneno ya kifungu hicho ni kwamba:
(i)
“Mamlaka ya ‘kujadili na kupitisha masharti ya Katiba
inayopendekezwa’ maana yake ni mamlaka ya kutunga na kupitisha Katiba
inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi wa Tanzania ili
kupigiwa kura ya maoni;
(ii) “Mamlaka hayo
yatatekelezwa kwa kutumia Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge
Maalum na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Katika kufanya
hivyo, Bunge Maalum linaweza kuboresha na/au kurekebisha Rasimu ya
Katiba. Mamlaka hayo yanamewekewa mipaka, kama ilivyokuwa kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, na tunu na maadili ya taifa yaliyopo kwenye
kifungu cha 9(2) cha Sheria;
(b) “Mahakama haina mamlaka
ya kuamua aina na upeo wa maboresho na/au marekebisho ambayo Bunge
Maalum linaweza kuyafanya kwenye Rasimu ya Katiba kwa sababu hilo ni
suala la kisiasa na wala siyo la kisheria, ilimradi maboresho na/au
marekebisho hayo hayaendi kinyume na matakwa ya kifungu cha 9(2) cha
Sheria.”
Uamuzi huu ni muhimu kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu zifuatazo:
(1) Tangu kuanza kwa Bunge Maalum mwezi Februari mwaka huu,
kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya wajumbe wa UKAWA na wajumbe wa CCM na
mawakala wao katika Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Bunge Maalum kama
yalivyoainishwa kwenye kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Wakati UKAWA imeshikilia msimamo kwamba mamlaka ya Bunge Maalum
yana mipaka kisheria na Bunge hilo halina mamlaka ya kubadilisha misingi
mikuu ya Rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, CCM na mawakala wake
imeshikilia msimamo kwamba mamlaka ya Bunge Maalum hayana mipaka na
Bunge Maalum lina uwezo wa kufanya marekebisho au mabadiliko yoyote
kwenye Rasimu ya Katiba. Uamuzi wa Mahakama Kuu unathibitisha usahihi wa
hoja ya UKAWA kwamba mamlaka ya Bunge Bunge Maalum yana mipaka
kisheria;
(2) Kwa kusema kwamba Bunge Maalum lina
mamlaka ya kufanya maboresho na/au marekebisho kwenye Rasimu ya Katiba,
Mahakama Kuu imekataa dhana ya CCM na mawakala wake kwamba Bunge Maalum
lina mamlaka ya kubadilisha Rasimu ya Katiba. Amri ya Mahakama Kuu
haijataja kabisa neno ‘kubadilisha’ ambalo liliingizwa kwa nguvu kwenye
Kanuni za Bunge Maalum. Kwa maana hiyo, kanuni ya 3 ya Kanuni za Bunge
Maalum inayotafsiri neno ‘hoja’ kuwa ni pamoja na mamlaka ya Bunge
Maalum kubadilisha Rasimu ya Rasimu inakwenda kinyume na matakwa ya
kifungu cha 25 cha Sheria na kwa hiyo tafsiri hiyo ni batili;
(3)
Kama ilivyokuwa kwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi
ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu iliyokuwa
inahusu suala la mgombea binafsi, Mahakama Kuu ya Tanzania imekwepa
kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki kwa kufuata Katiba na Sheria za
nchi kwa kujificha nyuma ya kichaka cha ‘maamuzi ya kisiasa.’ Mamlaka ya
Bunge Maalum yamewekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mipaka yake
imewekwa na Sheria hiyo pia. Mahakama Kuu, kama ilivyo kwa Mahakama
nyingine zote, ilikuwa na wajibu wa kutafsiri Sheria hiyo kwa kutamka
bayana aina na upeo wa mamlaka ya kisheria ya Bunge Maalum kufanya
maboresho na/au marekebisho ya Rasimu ya Katiba. Badala ya kutekeleza
wajibu wake huo, Mahakama Kuu imekwepa lawama za CCM na mawakala wake
kwa kusema kwamba aina na upeo wa maboresho na/au marekebisho ya Rasimu
ya Katiba utategemea matakwa ya kisiasa, yaani ya CCM na mawakala wake,
badala ya kutegemea lugha ya Sheria yenyewe. Aidha, Mahakama Kuu
imekwepa lawama za UKAWA kwa kukubali hoja kwamba mamlaka ya Bunge
Maalum yana mipaka, hata hivyo bila kuifafanua mipaka hiyo;
KATIBA MPYA INATENGENEZWA KWA MTUTU WA BUNDUKI!!!
Hali ya kisiasa katika nchi yetu kwa sasa ni tete kwa kiasi kikubwa.
Nchi yetu sasa iko chini ya utawala wa kijeshi usiokuwa rasmi. Kila
mahali katika makao makuu ya mikoa, wilaya na majimbo, askari wa Jeshi
la Polisi wakiwa na mabomu na risasi za moto, magari ya deraya, farasi
na mbwa wametanda kila mahali ili kujaribu kuzuia maandamano na mikutano
ya wananchi wanaopinga mchakato wa Katiba unaoendelea.
Mjini
Dodoma, Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linatumiwa na Bunge
Maalum limezingirwa na vikosi hivyo vya Jeshi la Polisi. Katika hali
hii, ni wazi kwamba mchakato wa Katiba umekuwa mateka wa Jeshi la
Polisi, Bunge Maalum lenyewe ni mateka na Watanzania wote ni mateka wa
Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya mabavu. Katiba mpya inatengenezwa
kwa mtutu wa bunduki. Katika hali tete kama hii, kitu cha ajabu kabisa
ni kwamba Rais Jakaya Kikwete – kama ambavyo imekuwa kawaida yake sasa –
amekimbia nchi na kwenda Marekani kwa ziara ya wiki mbili.
Kama
ambavyo UKAWA imesema katika kipindi chote hiki, chochote
kitakachotokana na mchakato huu wa kimabavu hakitakuwa na uhalali wowote
wa kisiasa. Sasa, baada ya mabadiliko mbali mbali ya Kanuni za Bunge
Maalum kuruhusu uchakachuaji sio tu wa Rasimu ya Katiba bali pia
uchakachuaji wa maamuzi ya wajumbe waliobakia wa Bunge Maalum, ni wazi
pia kwamba chochote kitakachotolewa na Bunge Maalum kwa sura ya Katiba
inayopendekezwa kitakuwa batili kisheria vile vile.
Kwa sababu
hizo, tunawaomba Watanzania wote wenye nia njema na nchi yao kupinga
nchi yetu kugeuzwa kuwa dola ya kipolisi na nchi ili chini ya utawala wa
kijeshi usio rasmi. Tunawaomba wanachama na viongozi wote wa vyama vya
UKAWA kufanya maandalizi ya kupinga vitendo hivi kwa njia mbali mbali za
kidemokrasia. Aidha, wanachama na viongozi wetu wafanye maandalizi kwa
pamoja kwa ajili ya Uchaguzi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliotangazwa
kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo uwe ni fursa ya kwanza
ya kuiondoa CCM katika utawala wa nchi yetu kabla ya kuiondoa kabisa
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
-----------------------------------------------------------
Mh. Freeman Aikaeli Mbowe
MWENYEKITI MWENZA
Mh. Profesa Ibrahim Haruna Lipumba
MWENYEKITI MWENZA
--------------------------------------------------------------------
Mh. James Francis Mbatia
MWENYEKITI MWENZA
Never afraid to try on your own; No matter what, you can keep it real. Trust yourself...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?
Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...
-
Ee Mungu Mwenyezi uliyekubali Mwanao Yesu Kristu ateswe mpaka kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu naomba uwe nami. Ee Msal...
-
Josephine is passionate, dedicated, reliable, responsible, and hardworking. Team worker and able to face all challenging situations. Can ...
No comments:
Post a Comment