Mwanafunzi
wa Chuo kikuu huria cha Tanzania Bw. Mussa Omari (katikati) akiongea na
waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu tamko la kulaani kauli za
mwenyekiti wa chadema taifa za kuhamasisha uasi kwa njia ya maandamano,
wakati wa mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi
wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bw. Gulatone Masiga akitoa wito
kwa wananchi kuudumisha muungano wetu na kuacha kupelekwa na wanasiasa
wasio na misingi ya kidemokrasia.Kulia ni Mwanafunzi wa Chuo kikuu huria
cha Tanzania Bw. Mussa Omari.
Mwanafunzi
wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Theodora Malata akiwaeleza jambo
waandishi wa habari leo wakati wa Mkutano uliofanyika jijini Dar es
Salaam.
======= ======= ========
UMOJA WA VIJANA WAZALENDO WA VYUO VYA ELIMU YA JUU DAR ES SALAAM
TAMKO LA KULAANI KAULI ZA MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA ZA KUHAMASISHA UASI KWA NJIA YA MAANDAMANO.
Sisi ni vijana wasomi wazalendo kutoka
vyuo vikuu mbalimbali vilivyoko Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM); Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU); Dar es Salaam University
College of Education (DUCE); USTAWI WA JAMII; Chuo Kikuu cha Mtakatifu
John (St. John); Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM); Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT); Kampala International University (KIU); Dar es Salaam
Institute of Technology (DIT); Institute of Adult Education (IAE);
Tanzania School of Journalism (TSJ); College of Business Education
(CBE), Chuo cha Uhasibu (TIA) na Chuo cha kumbukumbu ya Mwl JK Nyerere.
Tunachukua fursa hii kulaani
vikali kauli zilizotolewa na Mh. Freeman Mbowe ambae ni Mwenyekiti wa
CHADEMA ya kutaka kuitisha maandamano ya nchi nzima bila kikomo pamoja
na kuhamasisha asasi nyingine za kiraia kufanya na kuratibu maandamano
kama hayo ya CHADEMA kwa ajili tu ya kupinga kuendelea kwa Bunge Maalumu
la Katiba.
Tunawaambia
watanzania wenzetu kuwa tumekerwa na kusononeshwa sana na kauli ya
kibabe ya kiongozi huyu wa CHADEMA ya kuhamasisha vurugu ambazo
tumezishuhudia zikisambaratisha umoja wa nchi nyingi na kuwa chanzo cha
vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo huwa haviishi na
hatimaye kuendelea kulipakazia Bara la Afrika kuwa halijastaarabika na
siasa za kidemokrasia. Tulimsikia akiahidi maandamano bila kikomo kwa
kibali cha polisi au bila kibali cha polisi mbele ya wajumbe ambao
wengine sio watanzania. Ndugu watanzania wenzetu, kauli kama hii haiwezi
kusemwa hata na Rais yeyote ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu anaeongoza kwa
kufuata misingi ya sheria na utawala bora, je Mh. Mbowe anapata wapi
uhalali na ujasiri huo?
Maana
Rais na Amiri Jeshi Mkuu ambae ni dikteta anaweza kusema lakini yule
anaetawala kwa misingi ya sheria, katiba na utawala bora kamwe hawezi
kusema kauli kama hizo. Maneno aliyoyasema Mh. Mbowe amejivalisha
madaraka zaidi hata ya yale ya Rais wetu ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa
Vikosi vya Ulinzi na Usalama. Lakini kwa mtazamo wetu ni kuwa Mh. Mbowe
amejivalisha UDIKTETA ambao unatakiwa kulaaniwa na kila mtanzania
aliyeko ndani na nje ya nchi hii. Uzito wa kauli zake haubebeki na mtu
yeyote kwenye taifa hili. Hatuna shaka kuwa ametoa kauli mbaya sana
kuliko zote za kisiasa ambazo zimewahi kusemwa majukwaani.
Watanzania
kwa ujumla wetu na makundi yetu tukikaa kimya bila ya kuzilaani na
kuzikemea vikali kauli zake, tutakuwa hatujitendei haki sisi wenyewe na
pia hatutavitendea haki vizazi vijavyo vya nchi yetu.
Ndugu
zetu watanzania, kama ambavyo yeye mwenyewe alisema kabla ya kutoa amri
kwa watu kuandamana kuwa anaamini watanzania wapo tayari kufanya
mageuzi ili chama chake kingie IKULU ya Magogoni. Hayo yatafanikiwa
endapo tu vijana wataacha uoga, maneno ambayo yanaashiria kutaka
kuchukua uongozi kwa nguvu bila kufuata misingi ya kidemokrasia
inayosimamiwa na serikali iliyo madarakani.
Sisi
umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam
tunasema kuwa uzito na ubaya wa kauli hizi unaonesha wazi kuwa Mh.
Freeman Mbowe hafai kupewa dhamana ya kuwa Rais wa nchi na Amiri Jeshi
Mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama na pia amedhihirisha kuwa CHADEMA
haina sifa ya kuiongoza nchi hii kwa sasa kwa kufuata misingi ya
demokrasia na kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa watanzania kwa
lengo la kudumisha umoja, na muungano wetu.Tunaomba watanzania mkumbuke
na mtilie maanani kuwa, Mh. Freeman Mbowe katoa kauli hizi akiwa raia tu
wa kawaida.
Je itakuwaje akiwa Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama wa nchi hii? Kwa
maoni yetu ni kuwa kwa upeo na mtazamo wa akili yake hakuna atakaebaki
salama ndani ya nchi hii kwa kuwa atatuingiza kwenye vita vya wenyewe
kwa wenyewe na pia atatuingiza kwenye vita na nchi majirani. Hafai,
hafai, hafai hata mara moja kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. Ndugu
watanzaia, hivi ni mtu gani anaeweza kuishi kwa amani na viongozi kama
Mbowe na wenzake wanaotumia ubabe kwenye maisha ya kawaida ya kila siku?
Na
hapa ndipo wanatuthibitishia kuwa Mh. Freeman Mbowe na Kikundi cha
viongozi wa chama chake wote karibu wameshindwa kuzichunga na kuziweka
pamoja familia zao na hatimaye zimesambaratika kwa ubabe huo huo, hivyo
hawataweza kutuongoza na kutuweka pamoja watanzania ili tuishi kwa
amani.
Ndugu
watanzania wenzetu tumebaini kuwa Mh. Freeman Mbowe na viongozi wenzake
wa CHADEMA wanatumia maandamano na damu za watanzania kutafuta fedha
kwa wafadhili wao ambao hawaitakii mema nchi yetu. Wakiaandaa
maandamano, wanapiga picha na kuwapelekea wafadhili wao, wanapata
fedha, wanajenga majumba na kununua magari ya kifahari na kusafiri
ulaya, marekani na familia zisizo rasmi kwa kujificha kwenye pazia la
DEMOKRASIA huku watanzania wakiendelea kuathirika na maandamano. Hapo
ndugu watanzania hakuna DEMOKRASIA bali tunaona DOMO-KRASIA na
BONGO-KRASIA, yaani wanatumia
ulimi na akili ndogo za kitoto kujinufaisha na familia zisizo rasmi kwa
siasa za ulaghai, ghilba, fitina, majungu, choyo, chuki, usanii wa
kisiasa na uhaini alioutangaza Mh. Mbowe.
Ndugu
zetu watanzania, fahamuni kuwa Mh. Freeman Mbowe, Dk. Wilbroad Slaa,
Tundu Lissu, Godless Lema, Mchungaji Peter Msigwa, Hezekiah Wenje na
wengine wana familia. Swali je mmeshawahi kuwaona wake, watoto, na ndugu
zao wa karibu kwenye maandamano yoyote yale waliyowahi kuyaandaa? Siku
zote huwaambia watu wao hao bakini majumbani mtadhurika.
Pale
damu za watanzania zinapomwagika kwenye maandamano baadae huwa
wanajifungia na kushangilia ushindi mkubwa wa kuvuna mabilioni ya fedha
za kigeni, kwa kuwa huwa wanapiga picha
matukio hayo na kwenda kuonesha wafadhili wao kwa taswira kwamba
demokrasia inanyanyaswa. Wanakinga mabilioni ya fedha za kigeni wanatia
kwenye akaunti zao, wanagawana, na mambo yao yanaenda sawasawa, huku
watanzania wengine wakiwa wana vilio vya kupoteza ndugu na baba zao,
waume, wake, wapenzi/wachumba, na watoto wao na kadhalika. Swali kwa
nini hawaoni umuhimu wa kujali utu, ubinadamu na uhai wa watanzania
wengine?
Sisi
umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam
tunapenda kuwahakikishia kuwa thamani ya maisha ya watanzania wote au
hata kwa mtanzania mmoja ni kubwa sana kuliko hiyo katiba mpya
wanayoidai. Tunawaomba watanzania wenzetu msikubali kufanywa kama mbuzi
wa kafara na watu wenye tamaa, pupa, ulevi, na uroho wa madaraka kama
hawa akina Mbowe na kundi lake.
Tusijiendee
tu kama kuku aliekatwa kichwa halafu akaachiwa atembee, na tusishikiwe
akili zetu kama za mbayuwayu kwani “Akili za Kushikiwa, ongeza na zako”.
Tuwakataeni wanasiasa uchwara waliofilisika kihoja na kutaka kuwatumia
ili kujinufaisha. Wanataka kutupeleka wapi? Ni dhambi isiyosameheka
kulitumbukiza taifa hili katika machafuko yenye majuto makubwa kama ya
Misri, Syria, Afrika ya kati, Libya, Sudan ya Kusini na kwingineko.
Tusikubali watupeleke huko, waacheni waende wenyewe kama wanaweza. kwani
nchi yetu ina mgogoro wa kisiasa?!!!!! Waulizeni wanataka nini?
Ndugu
watanzania wenzetu, tunaomba mjue kwenye nchi hizo hizo zenye
demokrasia pevu watu wa aina ya Mh. Freeman Mbowe (hasa kwa kauli zake
alizozitoa juzi tarehe 14.09.2014) wanaotaka kuvuruga na kuvunja misingi
mikuu ya utaifa wao (core values) kama vile amani, usalama na umoja
huwa hawavumiliwi hata kidogo.
Sisi umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam tunaviomba
vyombo vyetu vya dola visizivumilie kauli kama hizi zilizotolewa na Mh.
Freeman Mbowe hata mara moja. Kwani vyombo vya dola vina dhamana ya
kulinda, kutunza na kuendeleza amani na utulivu wa nchi yetu. Umoja
wetu, kwa heshima na taadhima
kubwa, tunaviomba vyombo hivi kumchukulia hatua kali za kisheria Mh.
Mbowe kwa kauli hii ya kutishia uvunjifu wa amani kabla hajaiingiza nchi
yetu kwenye machafuko ya kisiasa.
Sisi
umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam
hatutaki kuona vijana wenzetu na watanzania wote kwa ujumla wakiathirika
kwa ujinga huo wa maandamano yanayofanywa mradi wa kutafuta fedha.
Kwani maandamano hayo yatawaathiri wana vyuo wa Dar es Salaam pamoja na
kuathiri shughuli nyingine za kiuchumi, na kijamii za wananchi wa
kawaida.
Kwa nini shughuli zetu na za wananchi zisimame kwa sababu tu ya machafuko ili Mh.
Mbowe apate picha za kwenda kuuza huko kwa wafadhili wao? Sisi umoja wa
vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam tulisikiliza na
kutazama hotuba ile kwa umakini wa hali ya juu, tunapenda
kuwathibitishia kuwa hotuba ile haikuwa ya kisomi, ilikuwa haijengi
chama chake wala ilikuwa haijengi nchi yetu isipokuwa ilikuwa ya kibabe,
ilikuwa ya kejeli, ilikuwa ya kichochezi iliyolenga kuvunja
misingi ya amani na utulivu wa nchi yetu. Ni matumaini yetu kuwa hata
kwa mwanafunzi wa shule ya msingi hawezi kujifunza kitu chochote cha
maana kutoka kwenye hotuba ile. Hotuba ya Mh. Mbowe haiwezi kutusaidia
kujenga taifa lenye dira kwa vizazi vijavyo.
Mwisho,
Sisi kama umoja wa vijana wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu Dar es
Salaam, tunawataka watanzania wenzetu mzipime na kuzitafakari kwa makini
kauli za Mh. Mbowe, na kujiuliza je anafaa kuwa kiongozi wa nchi hii?
Asanteni kwa kutusikiliza,
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Imesomwa na Mussa Omari, Mwanafunzi OUT, kwa niaba ya umoja wa vijana wazalendo wa Vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam
Tarehe 17.09.2014 Sahihi………………………. Simu 0715632681



No comments:
Post a Comment