..."Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi
kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na
kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa
Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo
kutowezekana kabisa..."
Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es Salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:
Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es Salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:
Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo
ilikusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu
yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano
walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.
Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na
kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi,
picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni
katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za
Tume na maoni yote yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume
iliandaa rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kwa kuzingatia maoni ya wananchi.
Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda kizalendo na kwa
mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande
wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho
wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa
Katiba ni maridhiano na si jambo la masilahi ya kisiasa, bali ni suala
la masilahi ya wananchi.
Tunaamini kuwa kila mjumbe wa kamati ya kukusanya
maoni ya wananchi aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi
waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa
au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa
wakati wa zoezi hili.
Baada ya Tume kuwasilisha rasimu kwenye Bunge
Maalumu la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa
wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya
Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya
masilahi kwa wananchi, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa
yanadhihirisha hili:
Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa
bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii
imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na
kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na
ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona
Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa
mbalimbali ambazo wananchi hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha
baina ya kinachojadiliwa bungeni na kilichomo katika rasimu na
viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na
kwa masilahi ya nani?
Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia kanuni kama
ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya
Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora
ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa wabunge wa Chama Tawala
(CCM), badala ya kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa
Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya wananchi.
Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya
kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni
yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la
Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake
baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na
wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa Katiba ni matokeo ya tendo la
maridhiano na si suala la masilahi ya kikundi cha watu wachache.
Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK
unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi
kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na
uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na
masilahi ya chama tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache
wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya
Katiba Mpya kwa nia ya kulinda masilahi binafsi au ya makundi na
kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi
bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;
1.
Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi
kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya
Katiba kwa uwazi.
2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na
kudharauliwa na chama tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba
linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba na siyo kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.
3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili
kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano mwafaka, uchaguzi mkuu na
wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977
yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka
kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye
kuendelea na mchakato wa Katiba.
4. Kwamba baada ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza
shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa
kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na
kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi katika Bunge la
Katiba.5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko
katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa
kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni
wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba
inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa
nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali
yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na
wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa
rasmi.
Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote
wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba amani ya
nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa
kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe
ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali
yoyote inayoweza kuathiri mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.
Ifahamike kuwa wananchi wa Tanzania wako juu ya
Wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe
wananchi wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa
tu chama hicho kimeyapuuza na kimekataa maoni yao waliyotoa kwa dhati
baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.
“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu
zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa.
Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa;
watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia
Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga
mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano,
wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana
nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)
Ikumbukwe kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba bni waraka
halali na rasmi na ndiyo mawazo ya Watanzania na tunahimiza kuwa Katiba
ni ya wananchi na inahitaji maridhiano na sio ubabe.
Imetolewa na Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT) Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)
Imetolewa na Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT) Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)
No comments:
Post a Comment