MBUNGE wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), amemwomba Rais Jakaya Kikwete amnyang’anye ubunge Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia.
Mrema alitoa ombi hilo juzi mjini hapa, alipokuwa akizungumza katika
kikao kilichowakutanisha wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD) na Rais Kikwete kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa Bunge Maalumu la
Katiba.
Chanzo chetu cha habari kilichokuwa katika kikao hicho kilichofanyika
Ikulu ndogo eneo la Kilimani, kilisema Mrema kuwa alisema Mbatia ni mtu
hatari kisiasa na anatakiwa kuchukuliwa hatua na Rais Kikwete kwa kuwa
ameanza kampeni kabla ya wakati.
“Mrema jana (juzi) alikuwa mbogo kwa sababu alipopewa nafasi ya
kuzungumza, alimwambia Rais Kikwete amfukuze Mbatia katika ubunge kwa
sababu anafanya kampeni katika jimbo lake la Vunjo.
“Mrema alisema Mbatia ni hatari sana, akasema pamoja na kwamba anafanya
kampeni kabla ya wakati, anayemlaumu zaidi ni Rais Kikwete kwa sababu
ndiye amempa jeuri baada ya kumteua.
“Alipokuwa akisema hayo, Rais alicheka hadi akanyanyua miguu juu, yaani
ilikuwa ni burudani kwa sababu alikuwa akizungumza kwa msisitizo
akionyesha kukerwa na Mbatia,” kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Rais Kikwete alipokuwa akijibu malalamiko
hayo, alimtaka Mrema asiwe na wasiwasi kwa sababu wananchi wa Vunjo
wanamjua mbunge wao ni nani kati yake na Mbatia.
Alipozungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mbatia alikiri Mrema
kumshutumu mbele ya rais na kusema kuwa hiyo ni mara ya pili kufanya
hivyo hadharani.
“Ni kweli alilalamika kwa rais na hii ni mara ya pili, kwani mara ya
kwanza alilalamika Agosti 2, mwaka huu katika kikao cha TCD.
“Mrema namheshimu sana, namwomba aendelee kuwatumikia wananchi wa Vunjo,
ila kwa kuwa anazidi kunifuatafuata, Septemba 6, mwaka huu nitahutubia
mkutano wa hadhara huko Vunjo kueleza msimamo wangu,” alisema Mbatia.
Naye Mrema akizungumza na MTANZANIA kwa simu, alisema alilazimika
kumfikishia kilio chake Rais Kikwete kwa sababu ndiye alimteua Mbatia.
“Mbatia ni mtu hatari sana, yaani anakwenda jimboni na kuwaambia
wananchi mimi ni mzee, na kibaya zaidi anasema tumekubaliana nimwachie
jimbo.
“Kwahiyo, ni kweli nilimsema kwa Rais kwa sababu ananifanyia rafu kule jimboni, yaani huyo jamaa ni hatari sana,” alisema Mrema.
No comments:
Post a Comment