Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Rais Jakaya Kikwete baada
ya kuzomewa hadi kukatisha hotuba yake akipingwa na wananchi pamoja na
madiwani wa CCM wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma alipokuwa akitetea
kuwapo kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Lukuvi alikumbana na mkasa huo wakati akijibu hoja za Mbunge wa Dodoma
Mjini (CCM), David Malole ambaye alitaka CDA ivunjwe akiituhumu
kuwavunjia wananchi nyumba bila kuwatafutia mahali pa kuishi.
Hoja ya Malole kutaka CDA ivunjwe iliibuka katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kata ya Kikuyu, Manispaa ya Dodoma baada ya Rais
Kikwete kuzindua ujenzi wa Barabara ya Dodoma - Iringa.
Awali, mbunge huyo akitoa salamu kwa Rais Kikwete, alisema CDA imekuwa
ni kero kwa wakazi wa mji huu.
“Mheshimiwa Rais, ni bora CDA ikafutwa na ardhi ikarudishwa kwa
halmashauri kwa kuwa hakuna kitu kinachofanyika. Ipo miji mingi ambayo
haina CDA lakini imekuwa majiji. Leo hii zaidi ya miaka 40 CDA
imeshindwa kuufanya Mji wa Dodoma kuwa jiji,” alisema na kuongeza:
“Licha ya kuwa CDA jukumu lake ni kuhakikisha inapima viwanja na kupanga
ustawi wa mji lakini imeshindwa kufanya hivyo, jambo ambalo linawakera
wananchi wa Dodoma na kusababisha kukichukia Chama Cha Mapinduzi na
Serikali yao,” alisema.
Kutokana na hoja hiyo kushangiliwa na madiwani pamoja na wana CCM na
wananchi wengine, Malole aliendelea kufafanua kuwa suala la kupigania
wananchi wapate viwanja linamuweka katika hali ngumu kwa sababu
anatishiwa kuwa hatapata nafasi ya kugombea ubunge tena.
“Mimi nasema, ikimpendeza Mungu kuwa mbunge nitaendelea kuwa mbunge na
kama siyo mpango wa Mungu basi, kwani kuna propaganda nyingi juu yangu
lakini hiyo yote ni kutokana na kupigania wananchi wapewe haki zao,”
alisema.
Kuzomewa
Baada Malole kutoa madai hayo, Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya
CDA alilazimika kupanda jukwaani ili asawazishe kauli za mbunge huyo,
jambo ambalo liliibua zogo na wananchi kuzomea.
Zomeazomea dhidi ya Lukuvi ilitawala katika kipindi chote alichokuwa
jukwaani huku viongozi wa chama wakihaha kuwazuia wanachama na madiwani
wa CCM wasizomee bila mafanikio.
Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Lukuvi pale aliposema, “Mimi ni mdau
mkubwa wa CDA na ni kati ya watu ambao walishiriki kupeleka maendeleo
katika Mji wa Dodoma.”
Kauli hiyo ilisababisha madiwani pamoja na wananchi kuanza upya kumzomea
huku wakimtaka ashuke jukwaani kwa madai kuwa hana cha kuwaeleza hadi
wamwelewe.
Hali hiyo iliambatana na nyimbo zilizoanzishwa na madiwani, “CCM.. shuka
chini, CCM shuka chini” hali iliyomfanya Lukuvi kushuka jukwaani.
Baadaye Rais Kikwete akizungumza na wakazi hao, alitoa siku saba kwa
viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na mbunge kukaa na kutatua mgogoro huo
na aliahidi kukutana nao Septemba 8, mwaka huu.
Alisema migogoro haiwezi kutatuliwa katika mikutano ya hadhara, bali
vikao vya kazi. Aliwataka kukutana kuangalia ni jinsi gani watamaliza
mgogoro huo bila kuwa na fujo wala lawama.
No comments:
Post a Comment