HALI za waathirika wa kinywaji aina ya Togwa wa kijiji cha Litapwasi wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma inadaiwa kuwa bado ni mbaya kwani waathirika wa jinsia ya kiume wamedai kuwa hawana nguvu za kiume na wanawake wamekuwa wakienda kwenye siku zao bila mpangilio tofauti na awali.
Walisema kuwa wanashindwa kwenda hospitali kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu kwani wengi wao walilipishwa fedha nyingi walipo lazwa kwa mara ya kwanza mlipuko wakuharisha na kutapika ulipotokea Septemba 28 mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya waandishi wa habari waliotembelea kijijini hapo baada ya kupigiwa simu na baadhi ya waathirika hao walisema kuwa tangu waliporuhusiwa kurudi majumbani mwao hali zao bado hazijatengamaa kwani wamekuwa wakiumwa matumbo, kuuishiwa nguvu na mara nyingine wanapata kizunguzungu jambo ambalo limekuwa likiwapa hofu kubwa juu ya usalama wa maisha yao.
Omari Rashid (29)mkazi wa kitongoji cha msikitini kijijini hapo alisema kuwa tangu walipokumbwa na tatizo la kunywa togwa hali bado ni mbaya na kwamba hata nguvu za kiume hana kabisa na tumbo bado linaendelea kumuuma .
“Waandishi mimi kwa sasa sina tofauti na guta kwani nikilala sijisikii kitu chochote na badala yake nimekuwa nikilaumiwa na mke wangu lakini pia nikienda haja ndogo haitoki kama mwanzo jambo ambalo kwangu linaninyima raha kabisa ya maisha hivyo naiomba serikali ichuke jukumu la haraka kuja kutupima upya kwenye matumbo yetu wote tulioathirika na kunywa togwa.’’alisema Rashidi.
Silvia Komba (59) mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa tatizo kubwa alilonalo tangu alipokunywa togwa hiyo bado anaendelea kuharisha na kutapika hivyo ameiomba serikali kuchukuwa hatua za haraka kutafuta namna ya kumaliza tatizo hilo lililowakumba wanakijiji cha Litapwasi.
Naye Daflosa Kiwili (48) mkazi wa kijiji hicho hicho alielezakuwa yeye pamoja na familia yake wanaumwa na mume wake nguvu za kiume hana tangu alipokunywa kinywaji hicho wakati wa sherehe za kipaimara cha mtoto Dickson Nungu (14) mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Litapwasi .
Alisema kuwa hanashindwa kwenda hospitali yeye na familia yake kwa kuwa hali ya uchumi ni mbaya licha kuwa ndani ya nyumba yake anamahindi ambayo ameshindwa kuyauza kutokana na soko la mahindi kuwa ni gumu kwa wakulima wadogo na kwamba alipolazwa kwa mala ya kwanza katika hospitali ya misheni ya Peramiho alitozwa ghalama ya sh.100,000 licha kwamba serikali ilisema matibabu bule kwa waathirika wote wa togwa.
Taus Nginyani (59) mkazi wa kitongoji cha Ruvuma katika kijiji hicho cha Litapwasi alwaambia waandishi wa habari kuwa bado hali yake ni mbaya kwani mpaka sasa anaharisha na kutapika huku vidonda vikimtoka mdomoni ,sehemu za siri na tumbo bado linamuuma na nguvu za kufanya kazi hana pia kichwa na kifua kinamuuma mara kwa mara na kwamba anashindwa kwenda hospitali kwa kuwa hana fedha za matibabu hivyo ameiomba serikali iwapatie matibabu ya kina ili kubaini ndani ya matumbo yao kunatatizo gani.
Alfonsi Ngatunga (66) na Japhet Haule(78) wote wakazi wa kijiji hicho walisema kuwa bado wanamatatizo na miili yao bado haina nguvu kwani chakula wanakula tofauti na hapo awali kwani wamepoteza hamu ya kula hivyo ombi lao kwao serikali ione umuhimu wa kuwaletea huduma za haraka kijijini hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha msikitini Nasibu Kharid alisema kuwa kwa hivu sasa serikali inahitaji ichukuwe hatua za makusudi za kufika kwenye kijiji cha litapwasi na kukutana na waathirika wa togwa ambao hali zao bado zinazidi kudhoofika kwani waathirika wengi wanadai kuwa hawana nguvu za kufanya kazi.
Hata hivyo afisa mtendaji wa kijiji cha Litapwasi Ritha Nindi alisema kuwa tangu tatizo hilo limejitokeza kwenye kijiji hicho wananchi wengi bado wanaumwa licha ya kuwa kwa mara ya kwanza serikali ilichukuwa jukumu la kuwatengea eneo maalum la Liangweni ambako waathirika baadhi walilazwa na kupatiwa tiba na wengine walienda kutibiwa hospitali ya misheni ya peramiho,Hospitali ya Mkoa na kituo cha afya cha mji mwema kilichopo manispaa ya Songea.
Alisema kijiji cha Litapwasi kinavitongoji tisa ambapo alivitaja kuwa ni Litapwasi,Mbatamila,Mawaso,Mayukila,Namabalapi,Maiskitini,Ruvuma,manguchilo na Ngongano na kwamba kijiji hicho kinawakazi 3037 ambapo alitaja changamoto kubwa ni kwamba waathirika wengi bado wamekuwa wakilalamika kuwa hawana nguvu za kufanya kazi jambo ambalo linaleta shida hata kwenye shughuli mbali mbali za maendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti alipopigiwa simu na mmoja wa waandishi wa habari alisema kuwa sio jukumu la waandishi wa habari kupigiwa simu na waathirika wa togwa wanachopwaswa wakimbilie kwenye hospitali ambako watapatiwa matibabu.
Naye mganga mkuu wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma Dkt. Daniel Malekela alisema kuwa waathirika wa togwa ambao wanadai kuwa wanaendelea kuumwa wanatakiwa waende kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ambako watawakuta wataalam watakaoweza kubaini matatizo waliyonayo na si vinginevyo.
Mwenyekiti wa halimashauri ya Wilaya ya Songea vijijini ambaye pia ni diwani wa kata ya Mpitimbi ambako waathirika wa togwa wametokea aliwashukuru waandishi wa habari kwa kitendo cha kwenda kijijini hapo kwa lengo la kuwatembelea waathirika watogwa na kujuwa hali zao ambapo alisema kuwa tayari alishachukuwa hatua ya kuitisha mkutano wa hadhra ambao ulihudhuliwa na wanakijiji wote na waliazimia kusitisha sherehe zote ndani ya miaka 3 na kwamba atakayefanya sherehe kwa sasa ni lazima awe na kibali maalum toka polisi ambapo polis watahusika kusimamia sherehe hiyo na si vinginevyo
No comments:
Post a Comment