MHE JAKAYA MRISHO KIKWETE AMBAYE JANA ALITOA NISHANI KWA MUUZA CHIPS
Rais
Jakaya Kikwete jana aliwatunuku nishani Watanzania 28, akiwamo muuza
chips, Kassim Said Kassim (28), ambaye alipewa nishani na ushupavu
baada ya kupambana na kumdhibiti jambazi mwenye silaha.
Hafla ya utoaji wa nishani hizo ilifanyika jana jioni katika Viwanja vya
Ikulu na kuhudhuriwa na mabalozi na viongozi mbalimbali wa Serikali,
huku Kassim akiwa kivutio kutokana na idadi kubwa ya watu kushangazwa na
ujasiri wake wa kupambana na jambazi mwenye silaha.
Kijana huyo alikuwa wa mwisho kutajwa na baada ya mshereheshaji wa hafla
hiyo kueleza historia yake kwa kifupi kwamba alizaliwa mwaka 1986,
iliibuka miguno kutoka kwa wageni waliohudhuria hafla hiyo na
aliposimulia kisa chenyewe, kila mtu aliduwaa. Baadaye Kassim alimweleza
mwandishi wetu: “Nilikuwa nafanya biashara ya chips eneo la Buguruni
Malapa. Nakumbuka Julai 7, mwaka jana saa tatu usiku tulivamiwa na
jambazi aliyekuwa na bastola na kuanza kuwatishia wateja, akitaka
kupatiwa fedha na vitu mbalimbali.
“Kwanza alianza kuwashinikiza wateja wampatie fedha na alipoona hakuna
aliyemsikiliza, alichomoa bastola na kumtishia mmoja wa wateja, hapo
ndipo nilipoamua kupambana naye.”
Alisema alichukua chepe na kumpiga nalo mara mbili sehemu ya kichwani
hadi alipoanguka na kuzirai. Alisema baada ya hapo, alitoa ripoti polisi
ambao walifika na kumchukua.
Viongozi waliotunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano
Daraja la Pili ni Adam Sapi Mkwawa (marehemu), Erasto Man’genya
(marehemu), Pius Msekwa, Samuel Sitta, Francis Nyalali (marehemu),
Augustino Ramadhani, Timoth Apiyo (marehemu), Paul Rupia, Ali Salum
Ahmed na Mohammed Fakih Mohammed.
Waliopewa Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano Daraja la Tatu
ni Peter Kisumo, Anna Abdallah, Kingunge Ngombare-Mwiru, Isaack Sepetu
(marehemu), Alli Mzee Alli (marehemu), Brigedia Jenerali mstaafu Adam
Mwakanjuki (marehemu). Ali Ameir Mohamed, Al-Noor Kassum, Jenerali
mstaafu Ernest Kiaro (marehemu), Solomon Liani (marehemu), Augustine
Mahiga, Phillemon Mgaya, Ambindwile Mwaijande (marehemu) na Simeon
Mwanguku.
Waliopewa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano Daraja la Nne ni
Sophia Kawawa (marehemu), Haji Machano Haji, Johari Yusufu Akida na
Bendi ya Atomic Jazz. Jenerali mstaafu David Musuguri alipewa Nishani ya
Operesheni Safisha Msumbiji huku Kassim akipewa nishani ya ushupavu.
No comments:
Post a Comment