WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewasili jijini Doha, Qatar
jana usiku (Jumamosi, Desemba 20, 2014)
kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa
kuanza leo.
Lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kukuza mahusiano baina
ya nchi hizi mbili, kuangalia fursa za kiuchumi na miradi mikubwa inayoweza
kuzinufaisha nchi hizo na nje ya mipaka yake kwenye Ghuba ya Arabuni (Arabian
Gulf) na bara la Afrika.
Vile vile Waziri Mkuu anatarajiwa kutangaza fursa za
uwekezaji nchini Tanzania, fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji kwa
ajili ya sekta za uchimbaji gesi na mafuta, usindikaji mazao, uvuvi na mifugo,
ajira na uendelezaji miundombinu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo ya
kiserikali na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani.
Vilevile atakutana na Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii; Uchukuzi;
Miundombinu na Uwekezaji wa nchi hii. Naibu Mawaziri atakaokutana nao ni wa
Uchumi na wa Nishati.
Vilevile Waziri Mkuu amepangiwa
kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar Business
Community), wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar (Chamber of Commerce
of the State of Qatar) na pia atakutana na Watanzania waishio Qatar. Atatembelea
pia Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi ya
Qatar.
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na Maliasili
wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati, Bw. Charles
Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey Zambi.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
Bi. Halima Dendego, wabunge wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali na
wakuu wa taasisi za TPSF na TPDC.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, DESEMBA
21, 2014
No comments:
Post a Comment