Never afraid to try on your own; No matter what, you can keep it real. Trust yourself...
20 January, 2015
TAHADHARI YA MVUA KUBWA
KWA mara nyingine, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari ya kuwapo kwa vipindi vya mvua kubwa kwa siku kadhaa kuanzia jana katika maeneo ya ukanda wote wa pwani na mikoa ya Ruvuma, Morogoro na Pwani. Kama ilivyo ada na kawaida kwa mamlaka hiyo, kujali na kuthamini maisha ya wananchi na mali zao, juzi, TMA ilisisitiza kuwa mvua hizo zilitarajiwa kuanza kunyesha kuanzia jana. Pamoja na hadhari nyingine walisema vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24 ilitarajiwa kuanza kunyesha tangu jana katika maeneo yaliyotajwa. Nasi pia kwa mara nyingine tena, tunachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kwa mvua kuanza kuchukua tahadhari dhidi ya tishio hilo la kutokea kwa mvua kubwa. Tunasema hivyo huku tukifahamu kuwa wananchi wengi wamekuwa na kawaida ya kudharau taarifa za tahadhari zinapotolewa hadi pale wanapokuwa na majanga na baadaye kusukumiza lawama kwa serikali. Kwa vile TMA katika taarifa yao walisema mvua hizo zingeanza kunyesha jana, upo uwezekano kwa wakazi wa maeneo yaliyotajwa wakadharau hadhari hiyo endapo mvua hizo hazikunyesha, suala ambalo si sahihi. Kama inavyofahamika, majanga ya maji ni majanga ya hatari sana kwani huweza kutokea ndani ya muda mfupi na kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao ndani ya kipindi hicho hicho kifupi na mara zote jitihada za kupambana na maji hayo hukabiliwa na vikwazo vingi. TMA wanasema mvua hizo zitatokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la Bahari ya Hindi Mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar, na hivyo kusababisha ongezeko la unyevunyevu kutoka Misitu ya Kongo. Kwetu sisi tunaichukulia taarifa hii ya TMA kwa uzito mkubwa kutokana na ukweli kuwa ni taarifa inayotokana na vipimo vya kitaalamu ambavyo ni aghalabu sana kutoa matokeo yasiyo sahihi. Tunawasihi wananchi wa Lindi, Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Kisiwa cha Unguja na Pemba ambao ndio walio katika hatari zaidi ya kuathiriwa na mvua hizo, kuanza kuchukua kila aina ya tahadhari dhidi ya janga hilo na hasa wale wanaoishi kwenye maeneo kama ya mabondeni. Ni matumaini yetu kuwa hadhari hii pia itatumika kama motisha chanya kwa mamlaka zinazohusika na maafa kuanza kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na lolote litakalojitokeza katika wimbi hilo. Hakuna sababu tena kwa mamlaka hizo kusubiri hadi maafa kutokea ndio waanze kuchukua hatua za awali za kukabiliana na majanga ya maji ambayo mara zote yamekuwa ni makubwa na yanayoathiri sehemu kubwa ya jamii na miundombinu ya barabara, madaraja, umeme na mingineyo. Katika hili hakuna cha serikali, bali ni kila mtu kwa wakati wake kutimiza wajibu utakaoweza kumwokoa yeye mwenyewe, familia, ndugu na jamaa endapo balaa hilo litatokea. Tuchukue hatua kwanza badala ya kusubiri tatizo litokee.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?
Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...
-
Ee Mungu Mwenyezi uliyekubali Mwanao Yesu Kristu ateswe mpaka kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu naomba uwe nami. Ee Msal...
-
Josephine is passionate, dedicated, reliable, responsible, and hardworking. Team worker and able to face all challenging situations. Can ...
No comments:
Post a Comment