Chama
Cha Mapinduzi (CCM), kimejigamba kwamba kimeweza kuzuia ‘mafuriko’ kwa
mikono huku kikiwatakia kila la kheri baadhi ya makada wake
waliotangaza kutogombea kupitia chama hicho pamoja na wale waliokihama
na wanaotaka kukihama.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita waliokuwa madiwani jimbo la Monduli kupitia CCM
mkoani Arusha, walitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), huku wabunge wa viti maalum, Ester Bulaya na James Lembeli
aliyekuwa Mbunge wa Kahama wakitangaza kutogombea kupitia chama hicho.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akizungumza na mtandao huu jana
alisema CCM hakina uwezo wa kuzuia mtu anayetaka kukihama kwa sababu
hiyo ndiyo demokrasia.
Aidha,
Nape alisema vyombo vya habari vilimnukuu aliyekuwa mgombea urais
kupitia CCM, Edward Lowassa akisema kuwa watu hawawezi kuzuia ‘mafuriko’
kwa mikono na kwamba CCM imeweza kufanya hivyo, lakini habari hizo
haziandikwi.
Alisema
wanachama wanaotaka kuhama hawawezi kuzuiwa kwa namna yoyote na kwamba
hilo ni jambo la kawaida kufanyika kwa kada yoyote.
Akizungumzia
mchakato wa kumpata mgombea urais, ulivyokuwa ndani ya CCM, alisema
ulifuata utaratibu na kanuni zote na kwamba kama maneno mengi
yataendelea kusemwa atatoa video inayoonyesha kila kitu kilivyokuwa
ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC).
Kuhusu
makada waliokihama chama hicho na kujiunga na Chadema, Nnauye alisema
baada ya Baraza la Madiwani kuvunjwa hapakuwa tena na wawakilishi wa
aina hiyo.
Alisema
watu waliojiunga na Chadema huko Monduli mkoani Arusha hawakuwa
Madiwani kwa kuwa Baraza la Madiwani likishavunjwa hakuna tena nafasi
hizo za uwakilishi.
No comments:
Post a Comment