Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka
17, utawala wa Rais Barack Obama umeidhinisha baadhi ya shughuli za kiserikali
zisimamishwe kuanzia mapema leo baada ya Bunge la nchi hiyo kuikataa
bajeti yake, wakipinga mabadiliko ya kisheria ya sekta ya afya yaliyofanyika
hivi karibuni.
Huku matumaini ya suluhisho la
mtafaruku huo wa bajeti unaopambanisha wabunge wa chama tawala cha Democrat
dhidi ya Republicans yakizidi kufifia, wachumi na wataalamu wa uongozi wameonya
kuwa uamuzi wa kusitisha huduma ‘zisizo muhimu’ utaathiri uchumi wa Marekani
kwa kiwango kikubwa.
Wafanyakazi katika vitengo
mbalimbali vya serikali nchini humo waliodamkia maofisini leo alfajiri
wamejikuta wakirudishwa majumbani, huku karibu 800,000 kati yao wakiambiwa
wachukue likizo bila malipo mpaka muafaka utakapopatikana.
Wafanyakazi pekee watakaobakizwa ni
wale ambao shughuli zao haziwezi simama, kama vile madaktari na manesi,
waongoza ndege na wafanyakazi wa shirika la posta la Marekani.
Katika baadhi ya vitengo kama NASA –
inayofanya tathmini za usafiri wa kwenda sayari nyingine na anga za mbali –
zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi wote wamewekwa benchi katika kipindi hiki
cha mtafaruku wa bajeti.
Vilevile huduma za utoaji hati za
kusafiri na viza zinatarajiwa kusimama kwa kiwango kikubwa, na wasafiri toka
nchi nyingine wanaambiwa watarajie foleni ndefu kidogo katika vituo vya
uhamiaji kwa sababu wafanyakazi wengi wa kitengo hicho wamepumzishwa. (AFP)

No comments:
Post a Comment