Pichani: Mazishi ya dada aliyenyongwa
Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni jambazi anatafutwa na jeshi la polisi kwa
madai ya kufanya matukio mbalimbali ya kihalifu likiwemo tukio la hivi
karibu kumnyonga hadi kufa dada mmoja aliyetajwa kwa jina la Bahati
Husein mkazi wa Ulongoni A Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Akizungunza na 100.5 times fm, dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa
jina la Moshi Hussein alisema mtu huyo ambaye anatambulika kwa jina moja
la Godfrey, kabla ya kumuua dada yake alikuwa akimtamkia mara kwa mara
kwamba ipo siku atamuua.
“Tulikuwa tunaona kama utani maana alikuwa akisema suala la kumuua mara
kwa mara na siku chache kabla ya kumuua walikuwa na ugomvi ambapo
Godfrey alikuwa akimhisi dada yangu (ambaye kwa sasa ni marehemu)
anamahusiano na mwanaume mwingine hali iliyosababisha kaka aje na
kuwasuluhisha,” anaeleza Moshi huku akilia kwa uchungu.
Aliendelea kusema baada ya kusuluhishwa alionekana kuridhika na kumtaka
mkewe (marehemu) ampikie ugali ambapo marehemu alifanya kama
alivyoagizwa lakini usiku wake akamnyonga hadi kufa.
“Baada ya kumuua aliondoka usiku huo huo na asubuhi alipiga simu kwa
ndugu akisema eti anataka kuongea na mkewe kwa hiyo mtu aende ampe simu
ili wazungumze wakati anajua nini amekifanya!” Anasimulia Moshi.
Alipoulizwa wao walijuaje kama marehemu alinyongwa hadi kufa, Moshi
alisema baada ya kifo hicho walikwenda kuripoti kituo cha polisi
Stakishari ambapo kabla ya kujua kama ndugu yao ni marehemu walimchukuwa
na kumkimbiza katika Hospitali ya Amana ambapo mara baada ya madaktari
kumchukuwa vipimo iligundulika kuwa dada tayari alikuwa mfu.
“Tulipohoji chanzo cha kifo chake ndipo tulipoambiwa kwamba vipimo
vinaonyesha marehemu amenyongwa na shingo yake imevunjika mara mbili,” Alisema.
Aidha, akitoa historia ya mtu huyo anayetajwa kama jambazi sugu, kaka wa
marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Husein, alisema kabla
ya kutokea kwa tukio hilo Godfrey alikuwa akitumikia kifungo cha miaka
20 jela kwa kosa kama hilo (la mauaji) na aliachiwa huru mwaka jana kwa
msahama wa rais.
“Hadi anakuja na kuishi na dada yetu bwana huyu alikuwa jela akitumika
miaka 20 kwa kosa kama hili. Kwa sababu huyu jamaa (Godfrey) ni mtu
mwenye wivu sana na chanzo cha kufungwa miaka 20 ilikuwa ni baada ya
kumfumania mkewe na mwanaume mwingine gesti ambapo aliwauawa wote na
kesi kwenda mahakamani na kukutwa na hatia na kufungwa miaka hiyo 20 leo
kamuua dada yangu, ina niuma sana,” alisema Abdallah.
Aidha, mjumbe wa eneo hilo la Ulongoni A ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alithibitisha kutokea tukio hilo.
Jitihada za kumpata Kamanda wa polisi mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamanda
Mariathe Minangi hazikuzaa matunda baada ya simu yake kupokelewa na mtu
aliyejitambulisha ni mlinzi wake na kudai RPC yupo kikaoni. Jitihada za
kumtafuta RPC bado zinaendelea kwa ajili ya kutolea ufafanuzi tukuio
hili.
Kwa undani wa tukio hili, sikiliza kipindi cha Hatua Tatu Habari Ndio
Hii siku ya Alhamisi tarehe 26/06/2014 hapa 100.5 times kuanzia saa tatu
asubuhi hadi saa sita mchana.
No comments:
Post a Comment