26 December, 2014

UJENZI WA MABWENI SHULE ZA PEMBEZONI KUPUNGUZA MSONGAMANO WA WANAFUNZI MIJINI.

Jamii imetakiwa kuendelea  kuunga mkono juhudi za Serikali za ujenzi wa mabweni katika shule  za Sekondari  zilizoko pembezoni mwa miji hasa maeneo ya vijijini ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi mijini linalosababishwa na baadhi ya wanafunzi kushindwa kujaza nafasi wanazopangiwa   maeneo ya pembezoni mwa miji kutokana na umbali.


Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni jijini Dar es salaam na Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando wakati akizungumza na viongozi wa Elimu wa mkoa na walimu wakuu wa Shule za Sekondari za mkoa wa Dar es salaam wakati wa kikao cha Kamati ya Uchaguzi wa wanafunzi wa watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015.


Alisema  mwaka huu  mkoa wa Dar es salaam umekuwa na kiwango cha juu cha ufaulu  kitaifa kwa kuwa na wanafunzi wanaokidhi vigezo vya kuendelea na masomo ya sekondari kwa kiwango cha asilimia 78 ukifuatiwa na mkoa wa Kilimanjaro ambao umepata asilimia 69.


Alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 60,709 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka huu , wanafunzi 59,577 ambao ni sawa na asilimia 98.14  waliofanya mtihani huo, wavulana wakiwa 28,419 na wasichana 31,158.


Bi. Mmbando alibainisha kuwa  kati ya hao watahiniwa 1,132  sawa na asilimia 1.86 katika mkoa wa Dar es salaam hawawakuweza kufanya mtihani huo kutokana sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo, ugonjwa na sababu nyinginezo.


Akizungumzia  kuhusu ufaulu wa wanafunzi hao kimkoa alisema wanafunzi 46,434 sawa na asilimia 78 walifaulu mtihani huo na kuufanya mkoa wa Dar es salaam kuongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu kitaifa wavulana 22,389 na wasichana 24,086.


Alibainisha kuwa wanafunzi 36,610 walichaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na shule mbalimbali za Sekondari za ndani na nje ya mkoa wa Dar es salaam na kufafanua kuwa wanafunzi 9824 waliobaki sawa na asilimia 21 ambao nao wamefaulu watachaguliwa katika chaguo la pili kufuatia baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na shule zisizokuwa za serikali na nafasi zao kubaki wazi.


Katika kufanikisha zoezi hilo Bi. Mmbando alieleza kuwa mkoa tayari umeunda timu tatu zitakazofuatilia idadi ya wanafunzi watakaoshindwa kufika katika shule walizopangiwa  kuanzia Januari 14, 2015 katika halimashauri za Temeke, Ilala na Kinondoni ili nafasi zao zijazwe na wanafunzi wengine.


Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mapunda akitoa tathmini ya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika nchi nzima mwezi Septemba mwaka huu alisema mkoa wake ulifanya vizuri kutokana na juhudi za walimu pamoja na wanafunzi kuuelewa vizuri mfumo wa ufanyaji mitihani uliotumika wa Optical Mark Reader (OMR).


Alisema kuwa wanafunzi wa shule 506 za jiji la Dar es salaam walifanya mtihani walitumia mfumo huo kwa ufanisi mwanafunzi 1 alifutiwa matokeo yake kwa sababu za udanganyifu, 2 walipata alama 0  huku  wavulana 10 na wasichana 10 kutoka wilaya ya Ilala na Kinondoni waliibuka washindi wa nafasi 10 bora kitaifa.


No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...