10 January, 2015

RAIS DKT SHEIN AFUNGUA JENGO LA UPASUAJI VICHWA MAJI NA UTI WA MGONGO

        
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein amekemea tabia ya baadhi viongozi wa Taasisi  kuwazuia wafanyakazi wake kujiendeleza kielimu kwa lengo la kuongeza ujuzi na kuleta ufanisi.



Hayo ameyasema  Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja katika ufunguzi wa Jengo la Upasuaji Vichwa maji na Uti wa Mgongo ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya  miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.



Amesema tabia hiyo haifai kwani inarejesha nyuma maendeleo ya wafanyakazi na kuanzisha majungu, fitna  na uhasama katika taasisi  kati ya wafanyakazi wa kawaida na viongozi wao. Amefahamisha kuwa taaluma ndiyo inayopelekea ufanisi bora wa kazi na  kuleta mabadiliko kwa   kutoa huduma bora  na uhakika na kujenga taifa lililo imara.



“Mabadiliko hayaji   bila ya kuwa na taaluma  hasa katika sekta ya Afya hivyo viongozi  waruhusuni wafanyakzi wenu kupata elimu ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi”, alieleza Dkt. Shein. Amesema lengo la  Serikali ni kuipa hadhi Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya rufaa kwa lengo la kuimarisha huduma bora lakini  kutokana upungufu wa vitendea kazi mabadiliko hayo yanakuja hatua kwa  hatua.



Dkt. Shein ameeleza lengo la  Serikali ni kutoa huduma bora za afya kwa wananchi kwa kutumia  wataalamu wenye elimu na vifaa  vya  uhakika kadiri ya uwezo uliopo ili kuimarisha afya za wananchi.



Aidha Dkt Shein amesema jitihada kubwa zinahitajika katika kuandaa mipango madhubuti itakayosimamia kuendeleza kitengo cha  upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo kwa kutafuta wataalamu na madaktari bingwa watakaoendesha matibabu hayo.



Amesema kitengo  cha huduma ya upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo ni cha pekee kwa Afrika Mashariki na Kati ambacho kitasaidia kupnguza gharama za usafirishaji wa wagonjwa wa matatizo hayo  nje ya nchi. 

Amesisitiza madaktari kuwafanyia wagonjwa uchunguzi wa kina kabla ya kuwapa  matibabu ili waweze kutoa huduma ya uhakika na  kujiepusha kubahatisha.



Aidha ameutaka uongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kukamilisha sheria na kuweka taratibu ili Hospitali hiyo iweze kujiendesha na kusimamia kazi bila kutegemea  Serikali kuu. “Nijukumu la uongozi wa Hospitali hii kuandaa mipango mizuri  itakayoweza kuiimarisha  ili lengo  la kujiendesha  liweze kufanikiwa”. Alisitiza Rais wa Zanzibar.



Mapema akimkaribisha Mgeni rasmi, Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman alisema kupatikana kwa miundombinu katika kitengo hicho ni kuleta maendeleo katika sekta hiyo na ameeleza kitatoa huduma ya uhakika.



 Jengo hilo lenye vyumba viwili vya upasuaji, wodi nne za kulaza wagonjwa na chumba cha mikutano  limejengwa kwa msaada wa Shirika moja la Hispania  na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na limegharimu zaidi ya shilingi Mill 600 ambapo asilimia 60 zimetolewa na wafadhili.

                                      

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

UKIONDOA DIPLOMA, DEGREE AU PHD ULIYONAYO, KICHWA CHAKO KINABAKI NA NINI?

Horace Mann - Binadamu wa kwanza kugundua wazo la elimu Albert Einstein aliwahi kuulizwa akili ni nini? What is intellect? Akasema akili ni ...